Njia 4 za kutibu Maumivu ya mgongo

maumivu ya mgongo

Mbadala ya Nyumbani kwa Maumivu ya Mgongo

Maumivu ya mgongo ni mojawapo ya matatizo ya kiafya makubwa sana ambayo yanawaathiri watu wazee au wenye umri wa kati, lakini pia vijana ambao wanafanya kazi kwa masaa mengi mfano wabeba mizigo na bodaboda.

Maumivu yanaweza kuwa makali na kusababisha mateso, na kuzuia mtu kujikunjakunja mbele au kuelekea pembeni. Watu walio na uzito kupita kiasi wako katika hatari kubwa ya kupata maumivu ya mgongo. Wanawake wengi hupata maumivu ya mgongo wakati wa ujauzito. Maumivu ya mgongo yanaweza kukufanya ushindwe kazi zako za kila siku.

Nini chanzo cha maumivu ya mgongo

Kuna sababu tofauti za maumivu ya mgongo ikiwa ni pamoja na ajali, majeraha, misuli kuvutwa, mgandamizo kwenye maungio na matatizo ya diski. Kwa kiasi kikubwa aina nyingi za maumivu ya mgongo zinaweza kutibiwa nyumbani kwa kutumia njia rahisi za asili. Na hili ndio lengo la makala hii, fuatana nami ili uanze tiba haraka bila kupoteza pesa zako mahali.

1.Shugulisha mwili

Wengi wetu tunafikiri kwamba kupumzika kitandani kwa siku kadhaa kunaweza kuwa na manufaa kwa kuponya maumivu ya mgongo. Lakini madaktari wengi leo wanahimiza wanaosumbuliwa na maumivu ya mgongo kusimama na kuendelea kutembea huku na kule, na kufanya shuguli nyepesi.

Kulala au kukaa katika nafasi moja kwa muda mrefu sio tu kunaweza kuzuia mchakato wa kupata nafuu lakini pia kuzidisha hali ya maumivu. Shughuli endelevu na polepole kama kutembea na kujinyoosha zinaweza kuharakisha mchakato wa kupata nafuu.

2.Tumia Kifurushi cha Barafu

Kutumia kifurushi cha barafu kwenye mgongo unaouma kunaweza kusaidia kupunguza maumivu na kupunguza kero. Kifurushi cha barafu kitapunguza uwezo wa neva kutuma taarifa za maumivu kwa ubongo. Kwa matibabu haya, weka taulo nyembamba kwenye mgongo wako.

Chukua kiasi cha barafu na uiweke kwenye mfuko wa plastiki. Sasa weka kifurushi cha barafu juu ya taulo hii kwa dakika ishirini na kisha kuiondoa. Baada ya dakika 30, rudia zoezi hili.

3.Tiba Maumivu ya mgongo kwa Masaji

Kupata nafuu kutokana na maumivu ya mgongo, paka mafuta ya mkaratusi au lavender kwenye mgongo wako. Mafuta haya yameonekana kuwa na ufanisi katika kuponya maumivu ya mgongo. Baada ya kupakaa mafuta haya, mwambie mtu akufanyie masaji kwa dakika 20 kisha pumzika uone matokeo yake mazuri.

Unaweza pia kutumia mafuta ya kitunguu saumu au mafuta ya mnanaa kupaka kwenye mgongo na kupata nafuu kutokana na maumivu. Mafuta ya kitunguu saumu yanaweza kutayarishwa kwa kukaanga punje 10-15 za kitunguu saumu katika mafuta ya olive au ya nazi kiasi cha mililita 50.

4.Kuoga Maji Moto

Endapo matibabu ya barafu hayapunguzi maumivu yako, jaribu kuoga maji moto ili kupunguza maumivu. Zama mwili wako kwenye chombo kikubwa kilichojaa maji moto kwa nusu saa, hakikisha maji yasiwe moto sana mpaka ukaungua. Joto litasababisha misuli kuwa laini na kupunguza kero. Wanawake wajawazito hawapaswi kutumia tiba hii; badala yake wanaweza kutumia chupa ya maji ya moto ili kupata nafuu ya papo hapo kutokana na maumivu ya mgongo.

Njia nyingine ya kutumia joto kwenye mgongo ni kwa kuzamisha taulo kwenye maji yenye chumvi ya moto. Kamua taulo kisha jikande mgongo wako.

Angalizo

Endapo umeshaanza tiba ya hospitali usikatishe njiani. Lengo letu siyo kukufanya uache matibabu ya daktari wako. Lengo letu ni kukusaidia upate nafuu wakati unajiandaa kwenda hospitali. Kama njia zote hizi hazijakupa matokeo mazuri, tafadhali nenda hospital mapema muone daktari. Yawezekana kuna tatizo kubwa kiafya linalohitaji uangalizi wa karibu na vipimo zaidi.